Ni June 12, 2022 ambapo Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa alikutana na vyombo vya habari Mkoani Dodoma.
Hapa nimekusogezea ufahamu alichozungumza Msemaji huyo juu ya sakata la Ngorongoro.
“Kuna jambo limejitokeza kule Loliondo, Serikali kule kama ilivyo kwenye maeneo mengine ya Hifadhi zetu Serikali inaendelea na uwekaji wa alama za mipaka kati ya eneo ambalo Wananchi wanalitumia na eneo la Hifadhi kwahiyo kilichotokea kule Loliondo nafahamu Waziri Mkuu ametoa juzi taarifa Bungeni na jana RC ametoa taarifa”- Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa
“Kule Loliondo Watu wamekwenda kuwashinikiza Wananchi waende wakafanye maandamano kwenda kuwafuata Watu ambao wanafanya zoezi na matokeo yake ni haya ambayo mmejulishwa, Wananchi waliohamasishwa wakaenda kuwavamia Maafisa ambao walikuwa wanaweka hizi alama na wakamjeruhi Askari mmoja na tumempoteza Askari mmoja kwasababu alichomwa na mshale kichwani, Serikali inasisitiza kinachofanyika Loliondo hakuna Askari aliyekwenda kumfukuza Mwananchi wa Loliondo aondoke kwenye eneo lake”- Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa
“Tunawasihi Wananchi wa Loliondo tuheshimu utaratibu kuwaingilia Maafisa wanaotekeleza majukumu yao sio sawa, jambo hili linafuatiliwa na wote wanaofanya uchochezi huu watafikishwa mbele ya mikono ya sheria, nawaombeni Waandishi wa Habari tusishiriki kwenye uchochezi wa aina hii”- Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa
“Tusichanganye kuna suala la Loliondo na Ngorongoro, kule Ngorongoro tumewaambia vizuri Wananchi tuna eneo Handeni kule Tanga wale Wananchi wanaotaka kuondoka wanaondoka kule akienda anapewa nyumba, eneo la kilimo na ufugaji, kwahiyo dhamira ya Serikali ni njema”- Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa