Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Taasisi za fedha katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta mapinduzi kwenye Sekta ya Kilimo nchini ili kuharakisha maendeleo ya Watanzania mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Waziri Hasunga ametoa pongezi hizo katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta iliofanyika katika viwanja vya Posta jijini DSM.
Waziri Hasunga amesema pamoja na Serikali kuweka juhudi kubwa katika kuboresha sekta ya kilimo nchini, ni dhahiri kuwa bado wapo wakulima, hususan wakulima wadogo, ambao wamekuwa wakifanya kilimo duni kutokana na wengi wao kutomudu gharama za uendeshaji wa kilimo cha kisasa.
Jambo ambalo linahitaji ushiriki wa Taasisi za Fedha na wadau wengine wa sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuwajengea uwezo kimtaji wakulima hao na kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo.
“Nikiwa Waziri mwenye dhamana ya kilimo nimefurahishwa sana na ushirikiano huu wa utoaji wa huduma za uwezeshaji wakulima baina ya Benki ya CRDB, uhusiano ambao unakwenda kuleta manufaa kwa wakulima kwa kuwawezesha kupata mikopo nafuu ya vifaa vya kilimo ikiwamo matrekta, power tiller, mashine za kuvunia na nyinginezo” Waziri Hasunga
Pamoja na matumizi ya zana za kilimo, Waziri Hasunga amewaomba wakulima kujikita katika kilimo cha kisasa kwa kuhakikisha wanaanza na utafiti wa masoko kabla ya kulima ili kujihakikisha uhakika wa kuuza mazao yao baada ya mavuno badala ya kuanza kulima bila kufahamu mahitaji ya soko na hivyo kuishia kutegemea Serikali katika kutafuta masoko.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameshauri Watanzania kujikita zaidi kwenye kilimo cha kisasa ili kuongeza tija na hivo kukuza kipato chao na taifa kwa kwa ujumla huku akisema Benki ya CRDB imejipanga kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa kwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa zana za kilimo.
“Kama unavyofahamu Mheshimiwa kuna Taasisi za fedha zaidi ya 58 nchini na kwa ujumla wao wanatoa asilimia 60 ya mikopo yote ya sekta ya kilimo wakati Benki ya CRDB pekee inatoa asilimia 40. Hii inadhihirisha adhma ya Benki ya CRDB ya kuunga juhudi za Serikali za kuwaletea Watanzania maendeleo kwa vitendo kwa kuzingatia kuwa sekta ya kilimo inatoa ajira kwa takribani asilimia 75 ya Watanzania huku ikichangia asilimia 28 kwenye pato la Taifa” Nsekela
ZITTO KABWE ATOA TAMKO RASMI SAKATA LA MGOMBEA URAIS TUNDU LISSU NA MEMBE