Rais William Ruto amewaamuru wakuu wa taasisi kuwaruhusu wanafunzi kufanya masomo bila kujali kama wamelipa ada au la.
Ruto alisema serikali tayari imetoa pesa kwa ajili ya masomo na ni ‘utovu wa maadili’ kwa wakuu wa shule kuendelea kuwahangaisha wazazi na wanafunzi kwa kutolipa karo.
“Tulitoa Sh62 bilioni mnamo Januari kusomesha wanafunzi wetu.
Lakini hata baada ya maendeleo haya kuna wakuu wa shule wanawaambia wazazi walipe karo kwa sababu serikali haijatoa pesa kwa shule,” Ruto alisema.
“Tunajua umuhimu wa elimu na tunataka watoto wetu wote waende shule, wasimamizi wa taasisi waache kutumia fursa ya mazingira magumu ya wananchi wetu kuwalazimisha wazazi kulipa ada ya shule kwa kisingizio kwamba serikali haijatoa fedha.
Ruto aliyasema hayo Jumapili alipowasili katika Shule ya Msingi ya MachakusI kwa mkutano wa maombi ya madhehebu mbalimbali katika kanisa la Machakusi ACK eneo bunge la Teso Kusini, Busia.