Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo katika maoni yake ya kwanza kuhusu kupitishwa kwa mswada huo, Jumatatu alisema bado hajaupokea na nchi hiyo haitarudi nyuma kwenye rekodi yake ya haki za binadamu.
Rais Akufo-Addo aliongeza kuwa mswada huo umepingwa katika Mahakama ya Juu. Maoni yake yanafuata yale ya Wizara ya Fedha ambayo ilimshauri rais kuacha kutia saini Mswada wa Haki za Kijamii na Maadili ya Familia (anti-L cGBTQ+) na bunge kuwa sheria.
“Nimegundua kwamba, leo, pingamizi limetolewa katika Mahakama ya Juu,” Akufo-Addo alisema katika taarifa yake. “Katika mazingira hayo, itakuwa vizuri sisi sote kushikana mikono na kusubiri uamuzi wa Mahakama kabla ya hatua zozote kuchukuliwa,” Akufo-Addo alisema.
Mswada huo uliopitishwa wiki iliyopita Jumatano umepangwa kuharamisha uendelezaji, utetezi, ufadhili na vitendo vya ushoga.