Nchi kadhaa barani Afrika zilikumbwa na hitilafu kubwa ya mtandao siku ya Alhamisi huku nyaya nyingi za mawasiliano chini ya bahari zikiripoti hitilafu, waendeshaji wa mtandao na vikundi vya kuangalia mtandao vilisema.
Mtandao wa intaneti umeripotiwa kukatika katika nchi kadhaa zikiwemo Afrika Kusini, Nigeria, Ivory Coast, Liberia, Ghana na Burkina Faso.
Kampuni ya kuchanganua mtandao ya Cloudflare iliripoti muundo katika muda wa usumbufu ambao uliathiri pakubwa angalau nchi 10 za Afrika Magharibi, zikiwemo Ivory Coast, Liberia, Benin, Ghana, na Burkina Faso.
Kilichosababisha nyaya za kusambaza huduma hiyo kushindwa kufanya hakijabainishwa.
“Inaonekana kuna usumbufu wa mtandao, unaoathiri kutoka kaskazini hadi kusini mwa Afrika,” ilisema Cloudflare Radar, ambayo inatoa taarifa juu ya miunganisho ya mtandao.
Kasi ya muunganiko wa intaneti nchini Ivory Coast ulipungua hadi karibu 4% Alhamisi asubuhi, kulingana na Netblocks, ambayo inafuatilia usalama wa mtandao na muunganisho wa intaneti.
Nchini Liberia kasi ya muunganiko wakati mmoja ilishuka hadi 17% wakati Benin ilikuwa 14% na Ghana 25%, Netblocks ilisema.