Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dkt. Benson Bana amethibitisha kuwa Watu wasiojulikana nchini Nigeria wamemteka nyara Mtanzania ambaye ni Frateri wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers), Melkiori Mahinini (27) ambaye ni Mzaliwa wa Parokia ya Kabanga Jimbo la Kigoma.
Mtanzania huyo alikamatwa katika Jimbo la Minna nchini Nigeria, August 03,2023 akiwa na mwenzake Raia wa Burkina Faso, Padri Paul Sanogo ambapo Watekaji wamedai Naira mil 100 (Tsh. mil 314.4) ili wawaachie huru wote wawili.
Akiongea na @AyoTV_ Dkt. Bana amesema “Tukio la kutekwa ni kweli limetokea tangu Aug 03 mwaka huu, sisi tunaokaa huku hatushangai ni uhalifu ambao sio Mgeni umeshazoeleka hapa Nigeria Watu kutekwa Nyara kisha Ndugu zao wanadaiwa kikombozi (pesa), wakishamteka Mtu wanatangaza wanataka kiasi fulani, na hawa walipowateka hawa walitangaza wanataka Naira mil 100 (Tsh. mil 314.4)
“Kwa kawaida wanateka sababu ya fedha, Ndugu yenu akitekwa mnajikusanya kuona mtaanzaje mazungumzo nao, watakuwa na Mawakala wao wanaoweza kuzungumza kisha Watu wanakombolewa, Kijana wetu huyu Shirika lake la Dini linaeleweka, sisi kama Ubalozi dhamana yetu ni kulifuatilia kwa ukaribu”
“Maisha ya Mtanzania popote alipo katika eneo letu la uwakilishi ni kipaumbele chetu namba moja, kwahiyo tunafuatilia kuona Vijana hawa wanakombolewa, visa vya Watu kukamatwa kuuawa vipo vingi Nigeria, Watekaji mara nyingi wanataka pesa na mkichelewesha wanaweza kuwadhuru ili kuwaonesha wapo serious”