Mtawala mpya wa kijeshi wa Niger alikashifu nchi jirani na jumuiya ya kimataifa katika hotuba ya kitaifa iliyoonyeshwa kwenye televisheni Jumatano usiku, na alitoa wito kwa wakazi kuwa tayari kulinda taifa.
Katika mojawapo ya hotuba chache kwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi tangu kutwaa mamlaka kutoka kwa rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa Niger wiki moja iliyopita, Jenerali Abdourahmane Tchiani alionya dhidi ya uingiliaji wa kigeni na uingiliaji kijeshi dhidi ya mapinduzi hayo.
Tchiani, ambaye anaongoza walinzi wa rais wa Niger, pia aliahidi kuweka mazingira ya mabadiliko ya amani kuelekea uchaguzi kufuatia kumwondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum.
Hotuba yake inajiri huku kukiwa na mvutano unaoongezeka wa kikanda huku jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS ikitishia kutumia nguvu za kijeshi ikiwa Bazoum hataachiliwa kutoka kifungo cha nyumbani na kurejeshwa kazini ifikapo Agosti 6.
Jumuiya hiyo imeweka vikwazo vikali vya usafiri na kiuchumi.
Tchiani alisema kuwa Niger inakabiliwa na nyakati ngumu mbeleni na kwamba mitazamo ya “uhasama na misimamo mikali” ya wale wanaopinga utawala wake haitoi thamani ya ziada.
Alivitaja vikwazo vilivyowekwa na ECOWAS kuwa ni haramu, si vya haki, ni vya kinyama na ambavyo havijawahi kushuhudiwa.
Mkutano wa siku mbili wa wakuu wa ulinzi wa jumuiya ya ECOWAS ulifunguliwa Jumatano katika mji mkuu wa Nigeria ili kujadili hatua zinazofuata.
Abdel-Fatau Musah, kamishna wa umoja huo wa masuala ya kisiasa, amani na utulivu, alisema mkutano wa Abuja utashughulikia jinsi ya “kujadiliana na maafisa katika hali ya mateka ambayo tunajikuta katika Jamhuri ya Niger.”
Vikwazo vilivyotangazwa na ECOWAS siku ya Jumapili vilijumuisha kusitisha miamala ya nishati na Niger, ambayo inapata hadi 90% ya nishati yake kutoka nchi jirani ya Nigeria, kulingana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati Mbadala.