Mamlaka mashariki mwa Uganda imewazuilia watu saba wa familia ya Kiislamu kufuatia tuhuma za kumpiga msichana wa miaka 18 ambaye inasemekana alihudhuria ibada ya kanisa, polisi wamesema.
Kulingana na taarifa za polisi, msichana huyo alichapwa viboko 100 kwa fimbo na mjombake, huku wajomba wengine watano wakimzuia wakati wa mateso hayo. Picha za kuhuzunisha za tukio hilo zilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii, na kusababisha shutuma kali kutoka kwa Waganda.
Familia hiyo, akiwemo shangazi mlezi mkuu, imezuiliwa kusubiri uchunguzi zaidi. Samuel Semewo, kaimu msemaji wa polisi mkoani humo, alisisitiza kuwa wanafamilia waliohusika watakabiliwa na mashtaka ya kushambulia au kutesa. Alitaja hali ya msichana huyo kuwa “amepona taratibu akisubiri uchunguzi wa kimatibabu” baada ya madai ya kushambuliwa.
Mwakilishi wa eneo la baraza linaloongoza la kitaifa la Waislamu alishutumu tukio hilo kama “la kinyama ,” akisisitiza kwamba vitendo hivyo haviendani na kanuni za Uislamu. Licha ya uchunguzi unaoendelea, familia bado haijatoa tamko kuhusiana na tuhuma hizo.