Visa vya Corona nchini Kenya vimeongezeka baada ya idadi ya wanaopima kuongezeka kwa kasi kufuatia mikakati mipya iliyowekwa, ambapo mtoto wa miezi sita ametajwa kuwa miongoni mwa walioathirika.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizotolewa na Serikali ya Kenya, hadi kufikia jana kulikuwa na visa 535 vilivyothibitishwa, watu 182 wamepona na kuna vifo 24.
Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mercy Mwangangi ameeleza kuwa katika visa vipya vilivyoripotiwa hivi karibuni, “kuna watu wenye umri kuanzia miezi 6 hadi miaka 60.”
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, majiji ya Mombasa na Nairobi ndiyo yaliyoendelea kuwa na visa vingi zaidi vipya.
Wiki iliyopita, Hospitali ya Nairobi ilitangaza kuanza kufanya vipimo vya corona ikiwa imewezeshwa kupima sampuli 900 kwa siku moja. Ilieleza kuwa gharama za upimaji ni Sh.10,000 za Kenya (Sawa na Shilingi 215,000) kwa kila sampuli.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Kenya iliyokaririwa na Citizen, vipimo vitachukua kati ya saa 6 hadi 24 hadi kupata majibu. Watakaokutwa na virusi vya corona watapaswa kukaa karantini ndani ya hospitali hiyo kama wataona inafaa, na Wizara ya Afya itawafuatilia kwa ukaribu.
“Kwa sasa hospitali ina uwezo wa vitanda 37 vinavyoweza kutumiwa na watu walioathirika na virusi vya corona kwa kuwapa nafasi nzuri, vitanda 12 kwa ajili ya watakaokuwa ICU lakini tuna mpango wa kuongeza,” taarifa ya Wizara ya Afya inaeleza.
Serikali ya Kenya imeongeza timu ya wataalam wa afya katika hospitali hiyo waliopewa mafunzo na wenye nidhamu ya kazi watahusika.