Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa mstaafu wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira amesema watoa huduma wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC wamefanya uzembe katika tukio la kifo cha mama mzazi wa mtangazaji wa kipindi cha Tanzania Yetu, Hoyce Temu baada ya eneo la mapokezi kushindwa kuchukua hatua za haraka kuokoa uhai wake.
Akitoa kauli hiyo wakati wa ibada maalum ya mazishi kama rafiki wa karibu sana wa marehemu iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Mnazi Mmoja Mkoani Kilimanjaro, Mama Mghwira alitoa kauli hiyo wakati akitoa neno la shukrani kwa maisha ya marehemu Sion Temu na kuwaasa watoa huduma wa KCMC kuzingatia utu na uadilifu katika kazi zao.
“Niseme neno moja kwa watoa huduma wetu katika nyanja mbalimbali kila kazi unayopewa, unayojipa, unayotumwa tuifanye kwa weledi, upendo na kwa uaminifu sana, hatuna baraka zingine za kuokota huku duniani isipokuwa kuhudumia watu kwa upendo” Mama Anna Mghwira.
Mama Anna Mghwira aliongeza kuwa kulikuwa na uzembe baada ya mgonjwa kufika hapo na kukaa kwa zaidi ya masaa mawili bila kupokelewa katika mapokezi hiyo ya wagonjwa KCMC.
“Hatutaki kulaumu lakini kwa kweli kulikuwa na aina ya uzembe ambao tunaweza kuuzungumza ni kwamba mtu ameletwa kwenye kituo cha Hospitali mahali anategemewa apokelewe, hakupokelewa nimemshusha mwenyewe kwenye gari baada ya masaa mawili” Mama Anna Mghwira.
“Hilo halikuwa sahihi awe alikuwa mzima awe alikuwa ameumia awe alikuwa ameshafariki hakuna sababu. Katika hilo niwaombe sana ndugu zangu Hospitali yetu ya KCMC tuwe makini sana na jinsi tunavyopokea, tunavyohudumia na tunavyowaacha wagonjwa wetu hata wafu wetu” Mama Anna Mghwira.
“Wote ni wa kwetu walio hai ni wetu na wasio hai ni wetu na ndio maana tunawalilia, tunawafurahia tunawashangilia na tunawasheherekea, kama yupo mwana KCMC hapaapeleke ujumbe dhidi ya mapokezi hiyo ya wagonjwa haitendi kwa weledi, naomba sana hilo lizingatiwe na sisi wote mahala pale popote tulipo tunapotoa huduma.” Mama Anna Mghwira.
Aidha, Mama Anna Mghwira alitumia wasaha huo kwa wana Kilimanjaro kujiandaa kumpokea Mkuu wa Mkoa mpya kama walivyompokea yeye na kukaa kwa miaka minne ndani ya Mkoa huo.
“Mama nimekaa nae kwa miaka hii minne na sasa siku yake ya mwisho ya maisha na mimi ni siku ya mwisho ya kazi, ni jambo jema sana, wakati naingia hapa niliingia tulikuwa tunamzika Mzee Ndesamburo, Mzee ambaye pia alikuwa rafiki yangu nimetengeneza marafiki wengi sana japokuwa nimeishi kwa muda mfupi sana hata uhusiano wangu na Hoyce Temu umeimarika zaidi kwa kweli baada ya kuja hapa” Mama Anna Mghwira.
“Namshukuru Mungu kwa haya yote na nawaahidi kabisa popote pale ninapoenda nyumbani kwetu nilipotoka, kwangu ninapoishi karibuni nitaendelea kuwaombea, kuwakumbuka na kuwaenzi sana sana. Asanteni Wachungaji kwa ibada njema na mafundisho mazuri Mungu atubariki sote, Amina” Mama Anna Mgwira.
Marehemu mama Sion Temu alifariki dunia Jumapili ya siku ya Mama duniani (Mother’s Day) dakika chache baada ya kuongea na binti zake kwa simu na kuwatakia heri ya siku hiyo na kuzikwa siku ya Jumamosi tarehe 15/5/2021 nyumbani kwake Moshi Mnazi Mmoja mkoani Kilimanjaro.