Mahakama Kuu ya Kenya imeongeza muda wa amri ya kuzuia kutumwa kwa polisi hadi Haiti au nchi nyingine yoyote ikisubiri kusikilizwa zaidi.
Mapema mwezi huu mahakama ilisema walalamishi hao wameibua masuala muhimu ya kitaifa na maslahi ya umma.
Kenya ilikuwa imejitolea kuongoza kikosi cha kimataifa kwenda Haiti kusaidia kukomesha ghasia za magenge. Pia iliahidi kupeleka maafisa wake 1000 kwa misheni hiyo.
Ekuru Aukot aliyekuwa mgombeaji urais na mmoja wa walalamishi alisema katiba hailengi kutumwa kwa polisi nje ya nchi.
Aliongeza kuwa atalishtaki Baraza la Mawaziri kwa kudharau mahakama baada ya wao kuidhinisha kutumwa licha ya agizo la mahakama.
Bunge litahitaji kuidhinisha idhini hiyo kabla ya kuanza kutumwa.
Hata hivyo, timu ya wanasheria wanaowakilisha bunge la kitaifa iliambia mahakama kwamba bunge hilo haliwezi kujadili suala hilo hadi maagizo yatakapoondolewa.
Haiti imekumbwa na ghasia za magenge kwa miezi kadhaa. Kumekuwa na visa 3000 vya mauaji na visa 1500 vya utekaji nyara kwa ajili ya fidia kulingana na Umoja wa Mataifa.