Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, Mungu yuko pamoja na nchi yake akionyesha kujiamini kwamba Moscow itashinda katika mzozo wake na Ukraine.
Putin alieleza hayo jana Alhamisi alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Uchumi la Eurasia (SEEC) huko St. Petersburg.
Alipoulizwa ikiwa anaamini kwamba mzozo wa Ukraine utamalizika 2025 kwa ushindi wa Russia, kiongozi huyo alisema: “Ninaamini Mungu. Na Mungu yu pamoja nasi.”
Katika mahojiano hayo, Rais wa Russia amepuuzilia mbali ripoti kwamba Marekani inapanga kupendekeza kusitishwa mapigano katika hali yaliyofikia kwenye mstari wa mbele wa vita, mkabala wa kucheleweshwa uanachama wa Ukraine katika katika shirika la kijeshi la NATO.
Putin alisema ucheleweshaji huo ulipendekezwa kwa mara ya kwanza na rais wa Marekani anayemaliza muda wake Joe Biden mnamo 2021, na akaongeza kuwa Washington ilitaarifiwa wakati huo kwamba hilo halikubaliki kwa Moscow.
“Tunajitahidi pia kuumaliza mzozo,” Putin alisema, akisisitiza kwamba “lengo nambari moja” la Russia kwa mwaka 2025 ni kufikia ushindi kwenye medani ya vita.
Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameapa kuitisha mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Russia na Ukraine ndani ya saa chache baada ya kuingia madarakani.
Ingawa amekataa kuzungumzia pendekezo lake lolote analokusudia kutoa, lakini vyombo vya habari vimenukuu vyanzo kadhaa ambavyo havijabainishwa hadharani kuwa pendekezo hilo linaweza kuhusisha kusimamisha mzozo huo, huku kila upande ukibaki na eneo na ardhi unalodhibiti kwa sasa.