Zaidi ya mwaka mmoja uliopita, polisi wa mji wa Georgia walipokea vidokezo kuhusu machapisho mtandaoni yaliyokuwa yakitishia shambulio la risasi shuleni. Ingawa walimhoji mvulana wa miaka 13, hawakupata ushahidi wa kutosha kumkamata. Jumatano, mvulana huyo alifyatua risasi katika shule ya Apalache High School, na kuua watu wanne na kujeruhi tisa, maafisa walisema.
Kijana huyo sasa ana umri wa miaka 14 na ameshtakiwa kama mtu mzima kwa mauaji ya wanafunzi wa Apalachee High School, Mason Schermerhorn na Christian Angulo, wote wenye umri wa miaka 14, pamoja na walimu Richard Aspinwall, 39, na Christina Irimie, 53. Maafisa wa uchunguzi wa Georgia walithibitisha katika mkutano na waandishi wa habari.
Takriban watu wengine tisa ikiwa wanafunzi wanane na mwalimu mmoja walikimbizwa hospitalini wakiwa na majeraha, lakini wanatarajiwa kupona, kwa mujibu wa Sheriff wa Barrow County, Jud Smith. Kijana huyo anatarajiwa kupelekwa kwenye kituo cha kizuizi cha vijana siku ya Alhamisi.
Akiwa na bunduki ya aina ya (AR) assault rifle, kijana huyo alianza kufyatua risasi shuleni baada ya wanafunzi wenzake kukataa kumfungulia mlango wa darasa la hesabu, alisema mwanafunzi mwenzake Lyela Sayarath.
Ingawa FBI ilikuwa tayari imepokea vidokezo vya vitisho vya shambulio hilo mnamo Mei 2023, lakini uchunguzi wa awali haukuleta ushahidi wa kutosha kwa hatua zaidi.
Sheria ya silaha imekuwa suala linalojadiliwa kwa hisia kali nchini Marekani, huku visa vya mashambulizi ya risasi shuleni vikizidi kuwa tatizo kubwa. Kisa hiki kimeongeza mvutano kuhusu udhibiti wa silaha, lakini bado kumekuwa na mabadiliko madogo katika sheria za kitaifa.