Jeshi la Polisi mkoani Pwani, linamshikilia mwalimu Evata Mboya wa shule ya msingi Mwendapole, Kibaha, akituhumiwa kumshambulia kwa fimbo mwanafunzi na kumsababishia maumivu makali ya kichwa.
Mwanafunzi huyo wa darasa la tano mwenye miaka 12 walipewa adhabu ya kuchapwa fimbo na wenzake ambao walikuwa wakipiga kelele darasani.
RPC Pwani, Wankyo Nyigesa amethibitisha kuhusu tukio hilo na kusema Mwalimu huyo alitoa adhabu kwa wanafunzi 15 waliokuwa wanapiga makelele darasani ambapo walipigwa fimbo tatu kila mmoja.
Alieleza, baada ya muda walimu wakiwa ofisini walishangaa kuona wanafunzi wengine wakiwa wamembeba mtoto huyo huku akilalamika maumivu makali ya kichwa hali iliyosababisha kumpeleka hospital ya Tumbi na hali ilizidi kuwa mbaya ambapo mtoto huyo alihamishiwa hospital ya Mloganzila kwa matibabu zaidi .
Wankyo alifafanua kuwa mtoto anaendelea na matibabu na mwalimu Evata anaendelea kushikiliwa na Polisi huku upelelezi ukiendelea kufanyika na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.