Mwanablogu wa Morocco amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa “kumatusi” kufuatia malalamiko kutoka kwa Waziri wa Sheria kuhusu machapisho yanayohusishwa na kesi kubwa ya ulanguzi wa dawa za kulevya, wakili wake amesema.
Mwanablogu Mohamed Reda Taoujini ambaye aliyekamatwa wiki iliyopita katika mji wa Agadir (kusini-magharibi), alihukumiwa siku ya Jumatano jioni kifungo cha miaka miwili jela na faini sawa na euro 1,830 kufuatia malalamiko mawili ya Waziri wa Sheria, Abdellatif Ouahbi, kulingana na wakili wake Redouane Arabi.
Waziri huyo alimshutumu mwanablogu huyo kwa kumkashifu katika video mbili alizorusha mtandaoni akihoji kuwa huenda anahusishwa na biashara kubwa ya dawa za kulevya, kesi inayojulikana kwa jina la “Escobar of the Sahara”, baada ya kukamatwa kwa maafisa wawili waliochaguliwa kutoka chama chake cha siasa, cha Authenticité et Modernité (PAM), kama sehemu ya uchunguzi.