Kada na Mwanachama wa CCM wilayani Muheza mkoani Tanga ndugu Hamisi Sadiki Rajabu ametoa Computer, Printer na Photocopy Machine kwa Shule ya Msingi Zirai iliopo Kata ya Zirai wilayani Muheza. Msaada huo unafuatia juhudi za Hamisi katika kuchangia miradi ya kijamii na kimaendeleo huko Muheza.
Akiongea na vyombo vya habari, Hamisi ameeleza kuwa “nimeanzisha slogan yangu ambayo ni muhezanamimi miminamuheza ambayo chimbuko lake ni kuunga mkono kazi kubwa na ya kihistoria inayofanywa na Mhe. Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuleta na kukuza maendeleo hapa Muheza.
Ninajaribu kuitafsiri kwa vitendo kauli mbiu hii ambayo inawaleta pamoja watu wa Muheza katika kushiriki katika maendeleo yao.
Nimeshiriki kwenye miradi mingi hapa Muheza na lengo la kutoa vifaa hivi ni kutatua changamoto za uandaaji wa mitihani pamoja na taarifa mbalimbali katika Kata za Zirai, Kwezitu, Misalai na Kata za jirani. Wamekuwa wakifuata huduma hizo Muheza mjini ambako ni takribani kilometa 60.
Hamisi ameeleza zaidi kuwa, anaandaa mradi mkubwa ambao utashuhudia Computer zikitolewa kwa Shule zote za Msingi na Sekondari wilayani humo.
Wananchi wa Muheza wamemzungumzia Hamisi kama kijana mwenye mtazamo na uchungu mkubwa juu ya maendeleo ya Muheza na kutoa rai wadau wengi wamuunge mkono ili kuiwezesha Muheza kukua kimaendeleo.