Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka Wasanii wanaotaka kutumia Sare za Jeshi kwenye kazi zao kufuata utaratibu wa kuomba kibali ili waruhusiwe kutumia mavazi hayo, huku likitoa siku saba kuanzi leo August 24,2023 kwa Wananchi kusalimisha mavazi ya Jeshi au yanayofanana na sare za Jeshi.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu JWTZ Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda amesema….“Tunatoa siku saba kuanzia leo iwe mwisho wa kuyavaa, kuyatumia au kuyauza, kwa wale Wasanii wao watafuata utaratibu wa kuomba kibali ili waruhusiwe kutumia mavazi hayo, baada ya siku saba atakayekutwa na mavazi hayo atachukuliwa hatua kali ambayo itakuwa fundisho kwa wengine”
“Mavazi yawasilishwe kwenye makambi ya Jeshi, Vituo vya Polisi au kwa Wajumbe wa Serikali za Mitaa, hatutokuuliza umeipata wapi na ukifika wakati wa chai tutakunywa nae chai pamoja, tunatoa siku saba kuyasalimisha na ambaye hatoyasalimisha atakuwa na nia ovu na dhamira mbaya na atakuwa na lake jambo, Waswahili wanasema Mwanakulitafuta Mwanakulipata, kwahiyo Mwanakulitafuta baada ya siku saba atakuwa Mwanakulipata”
“Zipo baadhi ya Taasisi zinazowashonea Watumishi sare za aina hiyo, wapo pia Wafanyabiashara wanaoingiza nchini mavazi ya aina hiyo na kuyauza kwa baadhi ya raia katika maduka au maeneo yao ya biashara, wapo baadhi ya Wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia wawapo kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu”
“Baadhi ya Watu wanatumia mavazi hayo kuwatapeli Wananchi kwa kujifanya Wanajeshi na wengine kufanya vitendo viovu huku wakidhaniwa kuwa ni wanajeshi kitendo ambacho ni kinyume na sheria za Nchi na hakipaswi kufumbiwa macho”