Kipo kisa kimoja kutokea nchini Uganda ambacho kimewaacha watu wengi midomo wazi baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 70 kujifungua watoto mapacha baada ya kupata ujauzito kupitia mfumo wa kupandikiza mbegu uitwao (IVF) na kuwa kuvunja rekodi ya kuwa mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi barani Afrika kujifungua, kwa mujibu wa hospitali alikopata watoto hao.
Kituo cha Kimataifa cha Hospitali ya Wanawake na Kituo cha Uzazi mjini Kampala, nchini Uganda kilisema Safina Namukwaya alijifungua mtoto wa kike na wa kiume.
“Kisa hiki hakionyeshi mafanikio ya matibabu pekee bali inaonyesha nguvu na uthabiti wa roho ya mwanadamu,” hospitali hiyo ilisema kwenye ukurasa wao wa Facebook, kufuatia mwanamke Namukwaya kujifungua kwa njia ya upasuaji mapema wiki hii.
Namukwaya alikiambia shirika la habari la NTV kwamba huu ni uzao wa pili ndani ya miaka mitatu, baada ya kujifungua mtoto wa kike mnamo 2020. Aliongeza kuwa alipata matatizo mengi wakati wa ujauzito, ikiwa ni pamoja na kutengwa na baba wa watoto wake.
“Wanaume hawapendi kuambiwa umebeba zaidi ya mtoto mmoja, tangu nilipolazwa hapa hajawahi kufika,” alisema Namukwaya nakuongeza kwa kusema hajui atawezaje kuwalea watoto hao lakini anafurahi kuwa nao baada ya miaka mingi ya kuvumilia unyanyapaa na kejeli kutokana na kukaa muda mrefu bila kuwa na uwezo wa kupata watoto.