Mwanamama tajiri wa Vietnam ambaye alipoteza rufaa yake dhidi ya hukumu ya kifo wiki iliyopita amekata rufaa ya kifungo cha maisha katika kesi tofauti ambayo alipatikana na hatia ya utakatishaji fedha, vyombo vya habari vya serikali vilisema Alhamisi.
Truong My Lan, 68, alipatikana na hatia mwezi Aprili ya ulaghai wa pesa kutoka kwenye Benki ya Biashara ya Saigon (SCB) ambayo waendesha mashtaka walisema aliidhibiti na kuhukumiwa kifo kwa udanganyifu wa jumla ya $27 bilioni.
Makumi ya maelfu ya watu waliokuwa wamewekeza akiba zao katika benki hiyo walipoteza pesa, jambo lililoshtua taifa la kikomunisti na kusababisha maandamano nadra kutoka kwa waathiriwa.
Lan alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, na mahakama iliamua wiki iliyopita hakuna msingi wa kumpunguzia kifungo — lakini akasema bado anaweza kuepuka hukumu ya kifo ikiwa atarudisha robo tatu ya mali iliyoibwa.