Mwanafunzi wa kike alivuliwa nguo zake nje ya chuo kikuu chake nchini Iran katika kile ambacho baadhi ya wanafunzi na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema ni maandamano dhidi ya kanuni kali za mavazi ya Kiislamu nchini humo.
Tukio hilo, lililotokea siku ya Jumamosi, tangu wakati huo limeenea, likiangazia sheria tata za hijab za Iran na jukumu tata la wale wanaoitwa “polisi wa maadili”.
Mwanamke huyo ambaye bado jina lake halijafahamika, alisindikizwa kwa nguvu ndani ya gari na maafisa wa usalama na baadaye kupelekwa katika kituo cha wagonjwa wa akili, kulingana na gazeti la Iran Farhikhtegan.
Video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kusambazwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International inaonyesha mwanamke huyo akiwa amekaa nje ya chuo kikuu akiwa amevalia nguo za ndani pekee na nywele zake zikiwa wazi.
Video nyingine inamuonyesha akitembea barabarani, bado yuko utupu, kabla ya kundi la wanaume kumzingira, kumfunga kwenye gari, na kuondoka.
Amnesty ilisema Jumamosi mwanamke huyo “alikamatwa kwa nguvu” baada ya kupinga “utekelezaji mbaya” wa kanuni ya mavazi katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad cha Tehran.
Mwanamke huyo aliwahi kunyanyaswa na wanachama wa Basij, kikundi cha wanamgambo wa kujitolea wa Irani, ndani ya uwanja wa chuo kikuu, kulingana na chaneli ya mtandao wa kijamii ya wanafunzi wa Irani, jarida la Amir Kabir. Ilidai wanachama wa kikosi hicho walichana hijabu na kurarua nguo zake.
Likiwanukuu watu walioshuhudia tukio hilo, shirika la habari la serikali la Fars liliripoti kwamba mwanafunzi huyo alivua nguo zake baada ya maafisa wawili wa usalama “kuzungumza naye kwa utulivu” na kumuonya kuhusu kukiuka kanuni za mavazi.
Mkurugenzi wa mahusiano ya umma wa chuo kikuu hicho alisema mwanamke huyo alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya afya ya akili.