Mwanamume anayejiita Nabii Ishmael alishtakiwa katika mahakama ya Zimbabwe Alhamisi, baada ya polisi kuvamia boma ambako alikuwa akiongoza dhehebu la kidini na kukuta watoto zaidi ya 250 wakiwa wamezuiliwa shuleni na kutumika kama vibarua vya bei nafuu.
Polisi pia waligundua makaburi 16 ambayo hayajasajiliwa, yakiwemo ya watoto saba wachanga, katika shamba hilo lililoko kilomita 34 (maili 21) kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Harare.
Ishmael Chokurongerwa na wasaidizi wake saba walishtakiwa kwa kuwatumikisha watoto na kuwanyima huduma za elimu na afya. Msemaji wa polisi Paul Nyathi alisema uchunguzi bado unaendelea na huenda mamlaka ikamfungulia mashtaka zaidi.
Viongozi wa madhehebu hayo pia wanatuhumiwa kwa kuvunja sheria zinazotaka vifo na mazishi kusajiliwa. Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba kulikuwa na karibu watu 1,000 wanaoishi kwenye shamba hilo kabla ya uvamizi huo.
Chokurongerwa, 56, na wasaidizi wake wataendelea kukaa rumande baada ya hakimu kusema katika kikao chao cha mahakama kuwa atatoa uamuzi kuhusu ombi lao la dhamana wiki ijayo. Hakuna hata mmoja wa wanaume hao aliyekuwa na uwakilishi wa kisheria katika kikao hicho na haikufahamika walikokuwa wakishikiliwa.
Watu hao walimsihi hakimu huyo kuwaachilia kwa dhamana, wakisema wao si watu wa jeuri na wana watoto wa kuwatunza ambao wangeteseka iwapo watafungwa gerezani.