Mahakama ya China imetoa hukumu ya kifo iliyositishwa kwa mtu mmoja aliyejeruhi zaidi ya watoto kumi na wawili kwa kugonga gari lake kwenye umati wa watu nje ya shule ya msingi katikati mwa China kwa kile kilichosemekana ni kutokukubaliana na talaka kati yake na mkewe.
Watu 30, wakiwemo watoto 18 wa shule, walijeruhiwa katika kisa hicho katika Jiji la Changde mnamo tarehe 19 Novemba. Lilikuwa ni shambulio la tatu kwa umati wa watu nchini China katika muda wa wiki moja.
Hukumu ya kifo iliyosimamishwa kwa Huang Wen inaweza kubadilishwa na kuwa kifungo cha maisha ikiwa hatatenda uhalifu mwingine katika miaka miwili ijayo.
Uamuzi huo hata hivyo ulizua ukosoaji mtandaoni, huku baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiishutumu mahakama kwa kuwa mpole Huang.
Katika taarifa, mahakama ilisema Huang alitekeleza shambulizi hilo ili kuonyesha hasira yake baada ya kukabiliana na hasara ya uwekezaji na migogoro ya kifamilia.
Hukumu hiyo iliashiria mara ya kwanza idadi kamili ya majeruhi kutoka kwa tukio la Changde City kujulikana. Machapisho mengi kuhusu hilo yamefutwa kutoka kwa mitandao ya kijamii
Baadhi ya waangalizi wametaja mashambulizi hayo kuwa ni ya kulipiza kisasi dhidi ya jamii. Wengine wanasema matukio haya yanasisitiza kukatishwa tamaa kwa baadhi ya watu kuhusu uchumi wa China.