Mwanamume mmoja amefariki baada ya kukohoa “lita za damu” kwenye ndege kutoka Bangkok kuelekea Munich, kulingana na maelezo ya abiria .
Raia huyo wa Ujerumani, anayesemekana kuwa na umri wa miaka 63, alionekana mgonjwa punde tu yeye na mkewe walipopanda ndege ya Lufthansa siku ya Alhamisi, kulingana na walioshuhudia.
Mwanamume huyo alikuwa akitokwa na jasho jingi na alionekana kushindwa kupumua – lakini mkewe aliwaambia wafanyakazi kuwa yuko salama na hali hiyo ilimpata kwasababu kuchoka baada ya kukimbia kuiwahi ndege, ripoti zinadai.
Abiria Martin Missfelder alisema hali ya mwanamume huyo ilidhoofika haraka baada ya ndege hiyo kupaa na alianza kutema damu kwenye mfuko – kabla ya kuanza kumtoka mdomoni na puani.
Aliambia chombo cha habari cha Uswizi Blick: “Ilikuwa hofu kubwa, kila mtu alikuwa akipiga mayowe.”
Bw Missfelder alisema mtu huyo alipoteza “lita za damu” na kuta za ndege zilitapakaa damu.
Wahudumu wa ndege walitumia takriban dakika 30 kujaribu kumfufua mtu huyo kabla ya kutangazwa kuwa amefariki.