Mwanamume mmoja wa Israel anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 40 katika gereza la Malaysia na kuchapwa viboko baada ya kufunguliwa mashtaka ya kusafirisha silaha na kumiliki risasi nchini humo, mwendesha mashtaka alisema Ijumaa.
Shalom Avitan, mwenye umri wa miaka 38, alikamatwa mnamo Machi 27 katika hoteli moja katika mji mkuu Kuala Lumpur ambapo inadaiwa polisi walimpata bunduki sita na risasi 158.
Avitan alikana mashtaka hayo baada ya kusomwa kortini siku ya Ijumaa. Anaendelea kushikiliwa na polisi.
“Ni kosa kubwa,” naibu mwendesha mashtaka wa umma Mohamad Mustaffa P Kunyalam aliwaambia waandishi wa habari ndani ya mahakama.
“Anakabiliwa na kifungo cha jela cha miaka 30 hadi 40 pamoja na kuchapwa viboko si chini ya sita za miwa.”
Polisi walisema hapo awali kwamba Avitan aliwasili Malaysia kutoka Falme za Kiarabu kwa pasipoti ya Ufaransa mnamo Machi 12.
Baada ya kukamatwa, aliambia mamlaka kwamba alikuja Malaysia kutafuta Mwisraeli mwingine kutokana na mzozo wa kifamilia.
Malaysia yenye Waislamu wengi haina uhusiano wa kidiplomasia na Israel na kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono utawala wa Palestina.
Waisraeli wanahitaji visa na kibali kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuingia Malaysia.