Lusius Msemwa Mkazi wa kata ya Makowo halmashauri ya mji wa Njombe kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo amelazimika kusimama mbele ya wananchi katika mkutano wa hadhara na kumhoji mbunge wa jimbo la Njombe mjini Deo Mwanyika juu ya masharti yaliyopo kwenye mkataba wa bandari baina ya nchi ya Tanzania na kampuni ya DP World.
Msemwa mbele ya mkutano wa mbunge Deo Mwanyika katika kata hiyo alipofika kwa ajili ya kushuhudia kuanza kutolewa huduma za afya kwa mara ya kwanza kwenye kituo kipya cha afya Makowo kilichojengwa kwa zaidi ya shilingi Milioni 600 fedha ambayo ni mapato ya ndani,wakati wa ziara yake ya kijiji kwa kijiji amesema wananchi wa jimbo hilo hawana nia mbaya ya kuipinga serikali yao lakini wamekuwa na shauku kubwa ya kuomba kujua masharti yaliyopo kwenye mkataba.