HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala iko mbioni kuanza kutoa huduma mpya ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk. Irene Kato, amesema hayo wakati wataalamu wa Bohari ya Dawa (MSD), wakiendelea kukamilisha ufungaji wa vifaa vya mahsine hizo.
Alisema hatua hiyo inafikiwa ikiwa ni jitihada za serikali kupitia Bohari ya Dawa kuwezesha ufungaji wa mashine za kisasa katika hospitali hiyo.
“Sisi wataalamu tunaamini hatua hii itawapunguzia adha wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo ambao walikuwa wakiifuata mbali,”alisema.
Alisema huduma hiyo inatarajia kuanza kutolewa baada ya MSD kukamilisha hatua za mwisho za ufungaji mashine za kisasa 10 za kusafisha damu katika hospitali ya Mwananyamala.
Alieleza kuwa, ufungaji wa mashine hizo ni muendelezo wa maboresho ya huduma za afya nchini yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Afya.
“Kabla ya kukabidhiwa mashine hizi kwa hospitali husika MSD kwa kushirikiana na wataalamu wengine watatoa mafunzo kwa watoa huduma wa hospitali lengo ni kuendelea kuhakikisha vitendanishi vya mashine hizi vinapatikana wakati wote ili kuepuka kukwamisha huduma,”alisema.