Mwanasoka wa zamani wa Zimbabwe Charles Yohane amefariki dunia nchini Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka 48 katika tukio linaloonekana kuwa la wizi wa gari.
Beki Yohane alikuwa kwenye kikosi cha Warriors kwa mechi yao ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2004.
Kufuatia kustaafu kucheza alikuwa akifanya kazi Johannesburg kama mkufunzi wa kandanda na dereva wa teksi.
Mwili wake ulipatikana Soweto siku ya Jumatatu, ingawa inaaminika alifariki Jumamosi usiku.
“Alitekwa nyara, walichukua gari lake na kumpiga risasi kichwani,” kaka yake Lewis aliwaambia waandishi wa habari.
Yohane alihamia Afrika Kusini kutoka Zimbabwe mwaka 1996 na kuichezea timu ya Wits inayoshiriki ligi ya daraja la kwanza, na kuwa nahodha na kuweka rekodi ya kucheza mechi 268 kutoka 1997 hadi 2006.