Mwanahabari wa China amefungwa jela miaka minne kwa kuripoti kutokea Wuhan wakati mlipuko wa Covid-19 ulipoanza, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya maelezo kuhusu kirusi kisichojulikana cha nimonia kujitokeza katika mji huo wa katikati mwa China.
Zhang Zhan ambaye ni wakili wa zamani, amehukumiwa katika mahakama ya Shanghai kwa madai ya “kuchochea ugomvi” wakati akiripoti matukio ya mwanzo ya mripuko wa corona.
Ripoti zake za moja kwa moja na makala zilisambazwa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii Februari, na kuwafikia maafisa nchini humo ambao mpaka sasa wamewaadhibu watu wanane waliofichua habari za kirusi hicho, wakati wakiendelea kupuuza ukosoaji wa serikali kuhusu namna serikali ilivyoshughulikia mripuko huo.