Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndugu. Paul Makonda amewataka Wananchi wa Pangani kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ujenzi wa Miundombinu ya barabara.
Mwenezi Makonda ameyasema hayo leo tarehe 20 Januari, 2024 alipofika kukagua ujenzi wa Daraja la Pangani na barabara unganishi.
Akizungumza mara baada ya kukagua, amewataka TANROADS kujenga uwezo wa makampuni ya ndani ilikusudi yapewe nafasi ya kupata kazi za nje ya Nchi.
Amesisitiza kuweka mkakati wa kuwalinda wazawa jambo litakalosaidia kuongeza mzunguko wa kukua kwa uchumi wa ndani na badala yake kutoweka mazoea ya kuwapa kazi ndogondogo haswa kwenye miradi mikubwa.
Vilevile, amehimiza kushirikisha wakazi wa eneo husika kwa miradi yote Nchi nzima kupata kazi kwa asilimia kubwa kwenye miradi hiyo ilikusudi na wao kupata Ajira za muda zitakazoweza kukuza na kuwainua kiuchumi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Kindamba amemueleza Mwenezi Makonda kuwa mradi wa barabara ya Tanga – Pangani – Sadani – Bagamoyo ulikuwa ni mradi wa muda mrefu lakini kwenye awamu ya sita ya serikali ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia umekuwa sio wa ahadi na badala yake ni utekelezaji.
Barabara hiyo ina urefu wa Km 50 kutoka Tanga – Pangani ambapo zaidi ya Tsh Bilioni 67 zinatumika kwa ujenzi huo.
Aidha, amesema Ujenzi wa daraja la Pangani unagharimu zaidi ya Tsh Bilioni 80 na kipande cha barabara cha kutoka darajani hadi pangani chenye urefu wa Km 95.
RC Kindamba ameeleza faida zitakazotokana na ukamilishwaji wa Daraja hilo ambapo amesema litapelekea kukuza uchumi na kuinua ukanda wa utalii wa nyika inayotokana na mto pangani pamoja na kupunguza muda wa safari.