Mwenge wa uhuru mwaka 2024 unaendelea kukimbizwa Mkoani Kagera ukiwa unapitia miradi mbalimbali ya maendeleo Mkoani humo.
Ukiwa Wilayani Kyerwa,pamoja na miradi mingine umefika katika Kiwanda cha kuongeza thamani ya zao la kahawa kinachomilikiwa na kampuni ya KADRES na kuweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho kinachoendelea kujengwa ambacho kitasaidia kuongeza thamani ya zao la Kahawa Mkoani Kagera.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho,Mkurugenzi mwenza wa Kampuni hiyo Leodgard Kachebonao amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 6 za kitanzania huku akiongeza kuwa kinatarajia kukamilika Desemba mwaka huu ambapo kitazidi kufungua fursa nyingi zaidi ikiwemo ajira kwa vijana.
Aidha Mwenge wa uhuru umetembelea na kuzindua mradi wa ghara moja na mashine za kukoboa kahawa katika Chama Kikuu cha Ushirika (KDCU) ambao umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1 za Kitanzania na mradi huu utasaidia kununua kiasi kikubwa cha kahawa ikiwa ni sambamba na kuongeza thamani ya zao la kahawa kwa mkulima huku ukiongeza ajira pia kwa Watanzania.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za mwenge Kitaifa 2024 Godfrey Mzava amewapongeza kwa uwekezaji huo Mkubwa uliofanyika kwa Wilaya hizo mbili na kuongeza kuwa uwekezaji huo utasaidia kukabiliana na changamoto ya magendo ya kahawa hususani wakulima wanaouza kahawa nje ya Nchi kinyume na utaratibu