Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Njombe Dkt.Scholastika Kevela ameitumia sikukuu ya mwaka mpya kurudisha tabasamu usoni kwa Amir Mtendwa mwenye ulemavu wa kupooza miguu.
Mtendwa ambaye ni mkazi wa Kata ya Uhenga wilayani Wanging’ombe amekuwa akiendelea kutaabika kutokana na hali yake ya ulemavu wa miguu aliyoipata tangu akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu wakati akianza kusimama.
Mwenyekiti Dkt.Scholastika pamoja na familia yake January 2 ametoa salamu za sikukuu ya mwaka mpya wa 2025 kwa kumkabidhi Amir Mtendwa zawadi ya kiti mwendo ili kumrahisishia kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Tunayemwenzetu mhitaji kutoka Uhenga,tunacho kiti mwendo kwa hiyo tunatoa zawadi yetu ya mwaka mpya kwa kuwa sisi tumejaaliwa kila kitu lakini mwenzetu amepunguakiwa kwa hiyo tunatoa hii sadaka ili naye aweze kufanya kazi”amesema Dkt.Scholastika Kevela
Kwa upande wake shangazi wa Amir Mtendwa amesema kijana huyo alipata homa kali na kulemaa tangu akiwa mdogo alipoanza tu kusimama jambo ambalo limekuwa likiwapa wakati mgumu lakini kwa kupata kiti hicho itakuwa msaada mkubwa kwa kijana wao na kumshukuru mwenyekiti kwa msaada huo.
Aidha,Mwenyekiti Dkt.Scholastika Kevela ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wadau na wananchi wa mkoa wa Njombe kuwa,watu wenye uhitaji wapo wengi hivyo ni Jukumu la kila mmoja kuhakikisha anarudisha Tabasamu na kuwafariji watu wa aina hiyo kwani ndio sadaka yenye kudumu hata baada ya maisha ya Duniani.