Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Mwigulu Nchemba ametoa onyo kwa watu wanaozusha taarifa za ugonjwa na vifo kwa baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii.
Mbunge huyo wa Iramba Magharibi (CCM) amevielekeza vyombo husika kuchukua hatua bila kusubiri mtu binafsi alalamike.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Dk Mwigulu amesema, “Taifa lipo kwenye msiba wa viongozi wetu waliotangulia mbele ya haki kwa mapenzi yake Mungu. Kumetokea tabia mbaya ya kuzushiana kwamba fulani anaumwa, na fulani naye anaumwa.”
“Mara nasikia fulani amekufa na fulani naye amekufa. Huku ni kukosa utu ni kuathiri maisha binafsi ya mtu, familia yake na kusababisha taharuki kwenye jamii. Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mitandao kinazuia watu kutoa taarifa za uongo. Nimeelekeza vyombo vyote husika kuchukua hatua bila kusubiri mtu binafsi akalalamike. Nani amekupa kazi ya kufuatilia afya za wengine na kuwa msemaji wa hali zao? Tuache tabia hii mara moja.” Mwigulu