Rais wa Zaianzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali iko tayari kupokea msaada wa chanjo COVID -19 pamoja na misaada mbali mbali ya kitabibu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).
Dk. Mwinyi amesema hayo Ieo Ikulu Jijini Zanzibar , alipokutana na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani, anaefanyia shughuli zake nchini Tanzania Dr. Tigest Ketsela Mengestu, aliefika kujitambulisha.
Amesema sekta ya Afya nchini ina mahitaji makubwa ili iweze kufanikisha lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo azma ya WHO kuendelea kuisadia Zanzibar katika nyanja mbali mbali, ikiwemo utoaji wa mafunzo kwa madaktari na wafanyakazi wa Afya pamoja na uimarishaji wa miundombinu ni jambo muhimu.
Alisema katika hatua ya kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi, kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo Bima ya Afya nchini.
Aidha, alisema kuna haja ya kuimarisha miundo mbinu ya huduma za Afya, hususa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja ambayo hivi sasa haikidhi mahitaji ya wakati katika utoaji wa huduma kutokana ongezeko la watu pamoja na ufinyu wa nafasi.
Alisema Hospitali hiyo yenye majengo ya kale, ina ufinyu mkubwa wa nafasi, ikiwemo uchache wa vyumba vya upasuaji hususan kwa magonjwa makubwa kama vile moyo pamoja na kuwa na wodi chache za kulaza wagonjwa.