Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema nguvu inayotumika kupambana na wabadhirifu wa mali za umma visiwani humo si nguvu ya soda na mapambano hayo ndio kwanza yameanza.
Kadhalika, amesema wizi, ubadhirifu wa mali za umma ni mambo aliyoyavalia njuga na hataki masihara na kusisitiza kuwa ataendelea kuondoa muhali ili wale wote wanaohusika au waliohusika kwenye ubadhirifu wachukuliwe hatua.
Dk Mwinyi aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari Tanzania kuhusu siku zake 100 madarakani.
“Mimi wale wenye makosa makubwa ndio nawataka kwa hivyo nimeshatoa maagizo kabisa kwenye vyombo vyote kwamba hakuna mdogo, hakuna mkubwa lakini hususani hawa wakubwa…kwa hivyo ni vyema tukapeleka nguvu kubwa kwenye watu tunaowadai pesa nyingi na hili litafanywa hivyo ili tuondokane na kutumia rasilimali zaidi ya kile tunachokidai,” Dkt. Mwinyi.
“Vita dhidi ya rushwa, ubadhirifu, wizi wa mali ya umma nimelivalia nguja, hatutaki masihara kwenye hili, nilisema wakati kampeni kuwa nitaondoa muhali hapa Zanzibar na kweli nimeondoa, kwa sababu nimechukua hatua kila penye kasoro, wengine walisema ni nguvu ya soda, lakini ndio kwanza nimeanza mtasikia mengi vita ya rushwa ni suala la kudumu,” Dkt. Mwinyi.
“Kuna watu wamesharudisha fedha, nimeambiwa na ZAECA katika orodha yao kuna watu wamerudisha fedha nilichowaambia ni kwamba, mtu aliyerudisha fedha kama ni kwa makubaliano arudishe halafu asishitakiwe basi angalau afukuzwe kazi. Huwezi kuwa na mwizi akarudisha basi aendelee, atakuibia tena,” Dkt. Mwinyi.
“Kwenye makosa yote ni sawa madogo na makubwa lakini nimeviagiza vyombo vyote kuweka nguvu zaidi kwenye makosa makubwa kwa tuelekeze nguvu huko kwa sababu wakati mwingine unaweka mkazo kwenye kosa dogo mtu anadaiwa shilingi elfu ishirini wakati kuna wengine wana kesi za mabilioni, lazima tuweke mkazo kwenye kesi kubwa ambazo hata gharama za kuziendesha zinawiana au fedha tunazodai ni kubwa zaidi,” Dkt. Mwinyi.