Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amechukizwa na usimamizi mbovu wa miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dkt. Leonard Akwilapo kupeleka Wataalamu watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi katika Wilaya hiyo.
Waziri Ndalichako amesema hayo baaada ya kukagua baadhi ya miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya Kiwango, majengo ya shule ya msingi ya mfano Bwega kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na Wizara, pia usimamizi mbovu kwa mafundi wazembe.