Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amewataka wakandarasi wote wanaotekeleza Mradi wa umeme Vijiji kupitia Mradi wa REA awamu ya tatu Mzunguko wa Pili, kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili kufikia lengo la serikali la kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote cha Tanzania kabla ya Mwezi juni Mwaka 2024.
Naibu Waziri Kapinga amesema hayo wakati wa kuwasha umeme katika kijiji cha Maseyu kata ya Gwata na kijiji cha Newland kata ya Mikese Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Amesema adhima ya serikali ni kufikisha huduma ya umeme kwa vitongoji vingine 60 vilivyopo katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ikiwemo maeneo ya migodi ya uchimbaji madini.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi you, Mkurugenzi wa Huduma ya Umeme Vijijini REA Mhandisi Jones Olotu amesema jumla ya shilingi bilioni 134.9 zimetolewa na serikali kukamilisha miradi ya umeme kwa Mkoa wa Morogoro, ambapo Wilaya ya Morogoro ikitengewa shilingi Bilioni 30, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki likitengewa Sh. Bilioni 16.1.