Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Uchukuzi Atupele Mwakibete ameiagiza mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini(TPA) kuhakikisha inaanza kutoa huduma kwa kutumia Bandari kavu kwa kuanza na Bandari ya Kwala ili kupunguza Shehena ya Mizigo inayosababisha msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mwakibete ameyasema hayo baada ya kutembelea na kukagua Bandari kavu ya Kwala ambayo Ujenzi wake umefikia asilimia 95, ambapo ujenzi wa Barabara ya zege Kutoka Vigwaza Mpaka Kwala yenye urefu wa kilometa kumi na tano na Ujenzi wa Reli inayoingia katika Bandari hiyo vimeshakamilika.
“Mpaka sasa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 80 kwenye ujenzi wa Bandari hii ya Kwala na miundombinu yake, hivyo naelekeza TPA anzeni kutoa huduma kupitia bandari hii mara moja ili kupunguza Mizigo na Maroli katika Bandari ya Dar es salaam ili muweze kuvutia watumiaji zaidi wa Bandari ya Dar es salaam na kuongeza mapato”
Pia Mwakibete amekitaka kitengo cha Masoko cha TPA kutumia fursa hii ya kuanza kutumika kwa Bandari kavu ya Kwala kuitangaza Bandari ya Dar es salaam pamoja na Bandari zilizo chini ya mamlaka ya Bandari Nchini Kitaifa na Kimataifa ili ziweze kupata wateja wengi zaidi, kwani Bandari hasa Bandari ya Dar es Salaam inamchango Mkubwa sana katika kukuza pato la Taifa.