Mamlaka ya magereza nchini Namibia imepiga marufuku kuajiri watu wenye tattoo zinazoonekana kama sehemu ya jitihada za kulinda heshima ya muonekano kwa viongozi wa magereza, gazeti la ndani linaripoti.
Hatua hii inachukuliwa ili kulinda sura ya magereza, kwani kumekuwa na wasiwasi kwamba baadhi ya tattoo zinazochorwa na maafisa wa magereza zinaweza kuhusishwa na magenge ya wahalifu, kulingana na jarida la Namibian Sun.
Kamishna mkuu wa Huduma za Marekebisho ya Namibia (NCS), Raphael Hamunyela, alisema tattoo zinazoonekana si taswira nzuri ya kazi hiyo.
“Unapokuwa afisa wa urekebishaji tabia , huwezi kuwa mwanachama wa kikundi chochote. Sisi ni watumishi wa kila mtu. Wakati mapigano ya magenge yanapotokea, afisa wa marekebisho [aliyejichora tattoo zinazohusiana na genge] anaweza kushambuliwa. Kwa sisi kuwalinda maafisa wa kurekebisha tabia na shirika, hakuna tattoos,” Hamunyela alisema. “Hatutaki maafisa wa kurekebisha tabia washambuliwe,” aliongeza.
Alisema sera ya uajiri nchini na kanuni za maadili zitarekebishwa ili kuhakikisha kuwa siku za usoni hakuna mtu mwenye tattoo zinazoonekana atasajiliwa katika NCS.
“Tatoo mpya ni kosa la kinidhamu,” Bw Hamunyela alinukuliwa akisema.
Majina ya maafisa wa urekebishaji walio na tattoos pia yatachukuliwa kwa uhifadhi wa kumbukumbu.