Mahakama ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, imemhukumu mkazi wa mtaa wa barabara ya Mbutu, Mohamed Ahmed (54) kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumtishia na kumtolea lugha ya matusi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Elimajidi Kweyamba, amedai mahakamani kuwa mshtakiwa, alitenda kosa hilo January 09, 2018, saa 1:05 usiku katika maeneo ya barabara kuu ya lami ya Igunga mjini.
Amedai kuwa mshtakiwa huyo alimtolea lugha ya matusi Mwaipopo wakati akitekeleza majukumu yake.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Igunga, Ajali Milanzi, Kweyamba amedai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo wakati Mkuu wa Wilaya akitekeleza agizo la upandaji miti kama lilivyotolewa maelekezo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani.
Mwendesha mashtaka amedai kwamba katika kosa la pili, muda huo huo na tarehe hiyo hiyo, mshtakiwa akiwa na nia ovu, alimtishia maisha kwa maneno Mkuu wa Wilaya kuwa atamwonyesha na atahakikisha anahama Igunga kwa kumfanyia kitu kibaya.
Hata hivyo, baada ya kusomewa mashtaka yote mawili, mshtakiwa huyo alikiri kutenda makosa hayo.
Kabla ya kutoa hukumu, Hakimu Milanzi amesema kwa kuwa mshtakiwa amekiri mwenyewe makosa, atatumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu gerezani, mwaka mmoja kwa kosa la kwanza na miwili kwa kosa la pili.