Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji (MoU) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) yanayotoa fursa kwa taasisi hizo mbili kuuza nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na mfuko huo katika makazi ya kisasa yanayofahamika kama Dk. Hussein Mwinyi yaliyopo eneo la Mombasa kwa Mchina Mwanzo, visiwani Zanzibar.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa leo kwenye Ofisi za Makao Makuu ya ZSSF Zanzibar yanatajwa kuwa yatafungua fursa mpya kwa wananchi wa Zanzibar, Tanzania Bara, na raia waliopo nje ya nchi ‘Diaspora’ kuweza kumiliki nyumba kwa gharama nafuu na kwa urahisi zaidi.
Katika hafla ya kusaini makubaliano hayo ilishuhudiwa Mkurugenzi Rasilimali Watu wa ZSSF, Saleh Daudi Makame na Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Binafsi wa NBC, Elibariki Masuke wakiziwakilisha taasisi zao kwa kusaini makubaliano hayo, zoezi ambalo pia lilishuhudiwa na maofisa wengine waandamizi kutoka taasisi hizo.
Akizingumzia hatua hiyo, Masuke, alisema kuwa makubaliano hayo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuboresha upatikanaji wa makazi bora nchini kupitia huduma zake.
“Makubaliano haya yanafungua mlango kwa wananchi wa vipato vya aina zote ndani na nje ya Zanzibar, kumiliki nyumba kwa urahisi zaidi. Ni hatua mpya na kimbilio sahihi kwa wale wote ambao wamekuwa na changamoto za kumiliki nyumba kwa muda mrefu,” alisema Masuke.
Kwa mujibu wa Masuke, kupitia mpango huo benki ya NBC itatoa mikopo ya muda mrefu yenye masharti nafuu ikiwa na ukomo wa kipindi hadi cha miaka 25 kwa wateja watakaokidhi vigezo na masharti ya kunufaika na mpango huo.
“Mikopo hii inaanzia kiasi cha milioni 20 hadi kufikia thamani ya Shilingi bilioni 1, hivyo inawagusa wanunuzi wa nyumba wenye hali zote kiuchumi wakiwemo hadi wanunuzi wa nyumba zenye gharama kubwa. Lengo letu haswa ni kuhakikisha huduma hii inawafikia wananchi wa vipato vyote, wakiwemo wale wa vipato vya chini, kati na hata vipato vya juu’’
‘’Kimsingi hiyo ndiyo sababu mikopo yetu imebuniwa ili kutoa unafuu wa kifedha kwa wateja wa aina zote na yeyote mwenye ndoto ya kumiliki nyumba anaweza kufaidika,” aliongeza Masuke.
Aidha, Masuke alibainisha kuwa mikopo hiyo itaambatana na bima maalum itakayolinda nyumba hizo dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo vifo, ajali za moto, tetemeko na majanga mengine ya asili.
“Endapo mteja aliyekopa nyumba kupitia mpango huu atafariki kabla ya kumaliza mkopo wake, bima itachukua jukumu la kulipa deni lililobaki, hivyo kuondoa mzigo na usumbufu kwa familia ya marehemu. Bima hii pia inalinda mali ili kuhakikisha nyumba hizo zinabaki salama dhidi ya athari zitokanazo na majanga ya asili’’ aliongeza.
Kwa upande wake, Makame alisema nyumba hizo zinahusisha ukubwa na sifa tofauti ikiwemo zile zenye vyumba viwili, vitatu hadi vinne huku akibainisha kuwa tayari baadhi ya nyumba zimeshauzwa huku nyingine bado zikiwa sokoni.
“Kupitia ushirikiano huu mpya na benki ya NBC tunaamini kwamba mikopo hiyo itasaidia kuuza nyumba zilizosalia kwa uharaka zaidi hatua ambayo italiwezesha shirika kurejesha fedha kiasi cha Bilioni 35 zilizowekezwa kwenye mradi huu ili kuimarisha mfuko wetu na hatimaye uweze kuendelea kulipa mafao ya wanachama wetu kwa wakati,” alisema Makame
Makubaliano hayo yanaweka msingi thabiti kwa maendeleo ya makazi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, huku NBC ikiendelea kujidhihirisha kama mshirika muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wote.