Vita vya Israel huko Gaza tangu shambulio la Oktoba 7 vimefufua msukumo wa kimataifa kwa Wapalestina kupewa taifa lao.
Norway, Uhispania na Ireland siku ya Jumanne zimekuwa nchi za hivi punde zaidi kulitambua taifa la Palestina, zikiachana na mtazamo wa muda mrefu wa madola ya Magharibi kwamba Wapalestina wanaweza tu kupata utaifa kama sehemu ya mazungumzo ya amani na Israel.
Hatua yao ambayo imeikasirisha Israel, inafikisha nchi 145 kati ya 193 za Umoja wa Mataifa ambazo zimetambua taifa la Palestina.
Zinajumuisha nchi nyingi za Mashariki ya Kati, Afrika na Asia, lakini si Marekani, Kanada, sehemu kubwa ya Ulaya magharibi, Australia, Japan au Korea Kusini.
Mwezi Aprili, Marekani ilitumia kura yake ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia nia ya Wapalestina kuwa nchi mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.