Rais William Ruto wa Kenya amesema kuwa, ni lazima hatua za kiubunifu na endelevu zibuniwe ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Rais Ruto amesema hayo alipozungumza katika kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na usalama wa chakula jijini Arusha, kaskazini mwa Tanzania.
Hatua ambazo Rais Ruto amesema zitachukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati ikielekea Dubai kwa mkutano kuhusu mazingira wa COP28 baadaye mwezi huu, ni kuwa na ubunifu katika uchukuaji hatua ambazo zitakuwa athirifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Ruto amesema Afrika itatumia na kuonyesha uwezo wake katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Miongoni mwa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaohudhuria kikao hicho ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Evariste Ndayishimiye (Burundi) na Salva Kiir (Sudan Kusini).
Wengine ni waziri mkuu wa Rwanda Edouardo Ngirente na Rebecca Kadaga, naibu waziri mkuu wa kwanza wa Uganda.
Mkutano huo umefanyika huku mataifa ya pembe ya Afrika ikiwemo Kenya na Somalia kwa sasa yanakabiliwa na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.