Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali imetangaza kwamba, kusimamishwa kwa huduma ya viza kwa raia wa Ufaransa ni hatua ya kulipiza kisasi, na baada ya nchi ya Mali kujua kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imeiweka Mali kwenye orodha ya maeneo mekundu.
Taarifa hiyo imesema, Ufaransa imesimamisha kutoa viza katika ubalozi wake mjini Bamako.
Mvutano katika uhusiano wa baadhi ya nchi za Magharibi mwa Afrika na Ufaransa umeongezeka kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Niger na kuondolewa madarakani rais wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum hapo tarehe 28 Julai. Bazoum anatambuliwa kuwa mtu mwenye uhusiano mkubwa sana na Ufaransa.
Serikali ya Mali tayari imefuta makubaliano yote ya ulinzi na Ufaransa na washirika wake wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya ushirikiano wa ulinzi yaliyotiwa saini mwaka 2014 na Paris.
Katika hatua nyingine ya kukabiliana na ukoloni mamboleo wa Ufaransa, asilimia 97 ya raia wa Mali wamepiga kura ya kuunga mkono kutotambuliwa tena Kifaransa kama lugha rasmi ya nchi yao.