Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameshiriki hafla ya utiaji saini wa Mikataba Mahsusi 3 ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam leo tarehe 22 Oktoba, 2023 Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.
Hapa nimekusogezea nukuu za Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa alichozungumza katika hafla hiyo.
“Meli nyingi husubiri nangani kwa muda mrefu kabla ya kuhudumiwa. Mpaka sasa tunazo meli 29 zinazosubiri kuingia bandarini. Lakini katika gati 12 ambazo tunazo, tuna meli 12 ambazo zilihudumiwa. Mheshimiwa Rais, wastani wa meli kusubiri nangani ni siku 5 kwa kiwango cha chini hadi siku 10 ikilinganishwa na bandari za wenzetu kama Mombasa ambao wastani ni siku 1.25 lakini kwa bandari ya Durban ni siku 1.6,” Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa.
“Pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za maboresho katika bandari ya Dar es Salaam, bado ufanisi wa utoaji huduma za bandari haujafikiwa viwango vya kimataifa. Hali ya sasa ya utendaji wa bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda” – Plasduce Mkeli Mbossa, Mkurugenzi Mkuu TPA
“Hili linatokana na kukosekana kwa uwekezaji mkubwa kwa muda mrefu ambazo zingeweza kupelekea kuongeza idadi ya gati katika maana ya kwamba tunazo gati 12 tu katika bandari ya Dar es Salaam. Lakini tunazo meli 30 ambazo zinasubiri kuingia. Lakini pia ni lazima uhudumie meli zile kwa wakati ili uweze kuingiza meli nyingine.” Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa.
“Athari za kutokuwa na ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na meli kusubiri muda mrefu nangani jambo ambalo linatokea mpaka sasa, ambapo kunasababisha kuongezeka kwa gharama za kutumia bandari ya Dar es Salaam” -Mkurugenzi Mkuu TPA, Plasduce Mbossa.