Viongozi wa nchi za Afrika Mashariki waliamua Jumanne kuongeza muda wa kikosi chao kilichotumwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika jaribio la kuleta amani katika eneo hilo.
Kufuatia mkutano wa kilele mjini Nairobi siku ya Jumanne, nchi saba za Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC) zilitangaza katika taarifa kwamba zimekubali “kuongeza muda wa mamlaka” ya kikosi hiki cha kikanda hadi Desemba 8.
Kikosi hiki cha wanajeshi elfu kadhaa kilitumwa mnamo Novemba 2022 mashariki mwa DRC, eneo ambalo limekuwa likikumbwa na ghasia kutoka kwa makumi ya makundi yenye silaha na waasi kwa karibu miaka 30. Lengo lake limepungua ili kuzingatia maeneo ya operesheni ya waasi wa M23 kaskazini na kaskazini magharibi mwa Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini.
Mustakabali wa kikosi hiki ulitiliwa shaka baada ya kukosolewa na Rais wa DRC Felix Tshisekedi, lakini EAC hatimaye iliamua mwezi Juni kuongeza muda wake kwa miezi mitatu.
Kundi la M23 linaloongozwa na Watutsi limeteka maeneo mengi katika eneo la Kivu Kaskazini tangu kuchukua tena silaha mwishoni mwa 2021 baada ya kukaa kimya kwa miaka mingi.
Kikosi cha EAC kimeteka tena baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na M23, lakini hadi sasa kimeshindwa kuzuia uasi huo.
Mara kwa mara DRC imekuwa ikishutumu nchi jirani ya Rwanda mwanachama wa EAC kwa kuwaunga mkono waasi, jambo ambalo Kigali inakanusha.