Waziri wa Rasilimali ya Madini na Nishati wa Afrika Kusini, Gwede Mantashe amesema, nchi za Afrika zinapaswa kukabiliana na tatizo la uhaba wa nishati na kuboresha kuhamia katika matumizi ya nishati ya uchafuzi mdogo ili kukuza uchumi.
Akizungumza katika Mkutano wa Mwaka 2023 wa Nishati ya Afrika ulioanza jana mjini Cape Town, Afrika Kusini, Bw. Mantashe amesema, zaidi ya Waafrika milioni 600 hawana umeme, jambo linalochangia maendeleo duni ya barani Afrika.
Amesema ni lazima kufanya kazi kwa pamoja na kukusanya uungaji mkono wa kifedha ili kutatua changamoto ya nishati barani Afrika, ambayo pia inajumuisha ukosefu wa miundombinu husika.
Ameongeza kuwa, uzalishaji wa umeme barani Afrika unapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya uchumi na jamii ya Afrika.
Mkutano wa 2023 wa Afrika Energy Indaba, ambao utakamilika siku ya Alhamisi, unatazamiwa kujadili masuluhisho ya kukabiliana na changamoto za nishati barani Afrika na jinsi ya kuendeleza mabadiliko kutoka kwa makaa ya mawe hadi nishati safi bila kuathiri uchumi wa nchi za Afrika, kulingana na mwandalizi.