Ndege iliyokuwa imewabeba mamia ya raia wa India waliokuwa wamezuiliwa kwa siku kadhaa kwenye uwanja wa ndege nchini Ufaransa kwa hofu ya ulanguzi wa binadamu imewasili nchini India.
Ndege ya kukodi ya Airbus A340, iliyokuwa ikisafiri kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwenda Nicaragua, ilizua shaka wakati wa kujaza mafuta.
Iliondoka ikiwa na abiria 276 lakini watu 25 wakiwemo watoto wawili walisalia Ufaransa baada ya kuomba hifadhi.
Washukiwa wawili wa usafirishaji haramu wa binadamu pia wamesalia nchini Ufaransa kwa uchunguzi zaidi.
Hata hivyo wawili hao waliachiliwa huru na mahakama. Ndege ya Legend Airlines ilitua Mumbai mapema Jumanne kwa saa za huko.
Picha zilizochapishwa na shirika la habari la ANI zinaonesha abiria kadhaa wakiwa wameketi kwenye viti vya plastiki kwenye uwanja wa ndege wa Mumbai baada ya ndege hiyo kutua.
Baadhi ya abiria walionekana wakitoka katika uwanja wa ndege lakini BBC idhaa ya Marathi inaripoti kuwa wengi wao walikataa kujibu maswali kutoka kwa vyombo vya habari.
Ndege hiyo hapo awali ilikuwa imezuiwa kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Châlons-Vatry, yapata kilomita 130 kutoka Paris, siku ya Alhamisi baada ya mamlaka kupokea taarifa isiyojulikana kwamba baadhi ya abiria wanaweza kuwa “waathirika wa biashara haramu ya binadamu,” waendesha mashtaka wa Paris walisema.