Ndege mbili za kibiashara zimepigwa risasi katika anga la Mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, wakati Ndege moja ya Spirit Airlines ilipokuwa ikijaribu kutua na nyingine ya JetBlue ilipokuwa ikiondoka kuelekea New York, kwa mujibu wa Ubalozi wa Marekani Nchini Haiti, tukio hilo limepelekea kusimamishwa kwa safari zote za Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Toussaint Louverture.
Ndege ya Spirit Airlines ilikuwa karibu kutua ikitokea Fort Lauderdale, Florida, wakati kundi la Wahalifu lilipofyatua risasi, na kumjeruhi Mhudumu wa Ndege, picha zilizozagaa Mitandaoni zinaonesha tundu la risasi lililoingia karibu na mlango wa nyuma wa Ndege na kusababisha uharibifu katika sehemu ya juu ya Ndege, baadaye Ndege hiyo ilielekezwa kutua katika Jamhuri ya Dominika kwa usalama wa Abiria.
Muda mfupi baada ya tukio hilo, Ndege nyingine ya JetBlue iliyokuwa ikiondoka Port-au-Prince ilipigwa risasi wakati wa kuondoka ingawa haikuripoti matatizo yoyote wakati wa safari na ukaguzi wa baada ya safari ulibaini kuwa sehemu ya nje ya Ndege hiyo ilikuwa imepigwa risasi, JetBlue imetangaza kuwa itasitisha safari zote kwenda Haiti hadi tarehe 2 Desemba huku uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea kwa kushirikiana na Mamlaka husika.
Kwa upande mwingine, kiongozi mpya wa mpito wa Haiti, Alix Didier Fils-Aime, ameahidi kushughulikia ghasia za magenge ya Waasi na kurejesha amani Nchini humo, Magenge hayo yanayodhibiti asilimia 80 ya Mji mkuu pamoja na Barabara kuu na miundombinu, mara nyingi yamekuwa yakilenga maeneo makubwa kama Viwanja vya ndege kwa lengo la kuchochea hali ya kisiasa.
Bwana Fils-Aime amesema kipaumbele chake ni kuimarisha usalama wa Watu na mali zao, pamoja na kurudisha uhuru wa harakati Nchini kote.