Ndege ya mizigo iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa imeanguka jana wakati ikitua kwenye uwanja mdogo wa ndege ulioko El-Barde, mkoa wa Kusini Magharibi nchini Somalia, na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wawili kujeruhiwa.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba misaada ya kibinadamu iliyotolewa na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) ilipotoka nje ya njia yake.
Umoja wa Mataifa umetoa salamu za rambirambi kwa familia na wafanyakazi wenzake na marehemu, na kuwatakia majeruhi kupona haraka.
Umoja huo pia umesema unafanyakazi pamoja na kampuni ya ndege iliyokodishwa, serikali ya Somalia na mamlaka za mkoa wa Kusini Magharibi kuchunguza tukio hilo.
Ajali hiyo imetokea wiki moja tu baada ya helikopta ya Umoja wa Mataifa kutua kwa dharura katika eneo linalodhibitiwa na kundi la Al-Shabaab mkoani Galmudug nchini Somalia.