Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) amewaagiza Maafisa Elimu Mikoa na Maafisa Elimu Sekondari wa Halmashauri nchini kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa miradi ya elimu usiku na mchana ili ikamililike ifakapo Agosti 2023 na kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha tano kupata miundombinu bora ya elimu.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo mkoani Tabora wakati akifungua Kikao kazi cha Maafisa Elimu Mikoa na Maafisa Elimu Halmashauri cha Tathmini ya Utekelezaji wa shughuli za elimu kwa mwaka 2022/23.
Amesema Serikali kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 7.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, vyumba vya madarasa na Matundu ya vyoo katika Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita.
“Tumtie nguvu Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo usiku na mchana na kuhakikisha inakamilika ili wanafunzi wa kidato cha tano watakaoripoti shuleni wawe na miundombinu ya kutosha kulingana na idadi yao” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI haitamfumbia macho yeyote atakashindwa kusimamia na kukamilisha miradi hiyo ifikapo mwezi Agosti 2023, kwani atakuwa ameshindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu.
Aidha, Ndejembi amesema Serikali kupitia mradi wa SEQUIP imetoa shilingi bilioni 21.18 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule mpya 212 za Sekondari za Kata pamoja na Shilingi Bilioni 48 kujenga Shule za Wasichana za Bweni za Mikoa katika mikoa 16.
Sanjari na hilo, amewataka Maafisa Elimu kufuata taratibu zilizobainishwa katika kusimamia shughuli zote za Elimu ipasavyo ikiwemo ujenzi wa shule mpya na miundombinu inayojengwa katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Charles Msonde amesema katika Kikao kazi hicho watajadili kwa kina kuhusu namna bora ya usimamimizi na Utekelezaji wa miradi elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ikamilike na kuleta tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa.